Kutokana na tafiti nyingi zilizofanyika, wataalamu  wameona kwamba kitendo cha mama kumnyonyesha mtoto kwa matiti yake huchangia katika kupunguza uwezekano wa mama kupata saratani (cancer) ya matiti.  (World Cancer Research Fund; http://www.wcrf.org/). Imeonekana kwamba sasa kuna uthibitisho mkubwa kuhusu jambo hili.

Tayari inajulikana kwamba mtoto anapata faida nyingi sana kutokana na maziwa ya mama, na sasa imeonekana pia kwamba mama anaponyonyesha mwili wa mama hupunguza aina ya vichochezi (hormones) ambavyo vina uhusika katika kusababisha saratani ya matiti. Kwa hiyo unapopata fursa ya kuwa na mtoto, jitahidi umnyoneshe mwanao kwa faida yako na ya mtoto wako. Inashauriwa kumnyonyesha mtoto bila kumpa kitu kingine chochote hata maji kwa miezi sita ya kwanza.

Mtoto aanzishiwe chakula cha nyongeza anapofikisha miezi sita huku akiendelea kunyonyeshwa hadi miaka miwili hata zaidi.  Pamoja na faida nyingi kwa mtoto, imezidi kuthibitishwa kwamba watoto walionyonyeshwa maziwa ya mama ipasavyo huzuia uwezekano wa kuwa na uzito uliokithiri (obesity) utotoni, ukilinganisha na watoto waliolishwa maziwa ya makopo (WCRF 2007; http://www.wcrf.org/research/expert_report/index.php ).  Tukumbuke kwamba uzito ulokithiri huchangia sana uwezekano wa kupata saratani na magonjwa mengine sugu.

Kumbuka: Mama kumnyonyesha mtoto kwa matiti yake humpunguzia uwezekano wa kupata saratani ya matiti.

Jipende na mpende mwanao! Ufunguo wa mtindo bora wa maisha upo mkononi mwako.

del.icio.us Digg Facebook Google Twitter Mail to a friend Thank you for sharing!