Nafaka zisizokobolewa (whole grains), aina mbali mbali za kunde na maharage (legumes) zimeonekana kuupa mwili afya bora na faida nyingi sana ikiwepo kuzuia baadhi ya saratani (cancer).  Tujizoeshe kula na tufurahie kula vyakula hivi.  Nafaka zisizokobolewa ni kama unga wa dona, mkate wa brauni (uliotengenezwa na ngano ambayo haikukobolewa sana), mchele wa brauni na ulezi, pia mtama (sorghum) au uwele ambao haukukobolewa. Jamii za mikunde zinahusisha maharage, kunde, mbaazi, njugu mawe, choroko, fiwi, dengu, njegee kavu nk.

Nafaka zisizokobolewa zina nyuzi-nyuzi ambazo wakati mwingine huitwa makapi-mlo (fiber) ambayo ni muhimu mwilini, pia huwa na virutubishi vingine ikiweko vitamin B ambayo mara nyingi huondolewa kwa kukoboa.  Aina za mikunde zina nyuzi-nyuzi, proteni kwa wingi na hazina wingi wa mafuta.  Vyakula hivi havina nishati-lishe (energy/calories) kwa wingi, hivyo unaweza kula na kushiba bila kuongeza uzito, pia hushibisha mapema.  Hata hivyo vyakula vyote ni muhimu viliwe kwa kiasi.

Nyuzi-nyuzi katika mlo zimeonekana kupunguza hatari ya kupata saratani ya utumbo mkubwa (colorectal cancer).  Hii ni kwa sababu husaidi kutoa mapema mabaki ya chakula ikiwa ni pamoja na chemikali ambazo huweza kuchangia kupata saratani.

Fanya nafaka zisizokobolewa kuwa sehemu ya milo yako kila siku.  Jizoeshe polepole utazoea hasa kwa sababu unaelewa faida zake.  Zaidi sana, wazoeshe watoto wako kula vyakula hivi, wao bado ni wadogo na wanahitaji sana kufanya kila linalowezekana kuzuia magonjwa na kurefusha maisha.  Mfundishe mtoto, mweleze kwa nini ni muhimu kutumia vyakula hivi, mshirikishe pia wakati wa kununua na kutayarisha, ataelewa.   Zoesha familia nzima kula vyakula hivi, epuka kununua nafaka zilizokobolewa, usikoboe mahindi, tumia aina mbali mbali za kunde au maharage kwa mara nyingi.

Jipende: ufunguo wa mtindo bora wa maisha upo mkoni mwako.

del.icio.us Digg Facebook Google Twitter Mail to a friend Thank you for sharing!
 Tagged as:
This entry was posted on Saturday, October 24th, 2009 at 12:48 pm and is filed under Kiswahili, Lifestyle. You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0 feed. You can leave a response, or trackback from your own site.