Hata tukiambiwa “kula chakula kupita kiasi kulisababisha kifo cha fulani”, hatuamini, au tukiamini, bado tunaendelea “kukupenda” na kula kupita kiasi! Sasa tutakutafutia mikakati!

Chakula ni kitu chochote kinacholiwa na kuupa mwili virutubishi. Nadhani kila mtu anapenda chakula, na kweli chakula ni kitu kizuri, tena huburudisha. Nakumbuka miaka kadhaa iliyopita nilikuwa naongea na kijana mdogo, mwenye umri kama miaka 18, tukazungumzia chakula.

Pamoja na mazungumzo mengine alisema hivi “ …..Kitu ninachofurahia kuliko vitu vyote ni kula, tena kula chakula kizuri kwa kiasi ninachotaka” Utaona hata hangependa kupimiwa, na nadhani japo watu wengine wanaweza kutofautiana nae kidogo, lakini ukweli mtu anapopata chakula anachokipenda anafurahia kula na asingependa kuwe na kipingamizi. Tatizo sasa ni kwamba tusipokuwa waangalifu chakula hicho ambacho tunakiona kizuri kinaweza kutuletea matatizo ya kiafya.

Ni muhimu kuwa waangalifu kwenye kiasi na aina ya vyakula. Hii ni kwa sababu uzito wa mwili uliozidi kiasi umethibitishwa kuwa na uhusiano mkubwa na magonjwa mengi sugu, zikiwepo cancer za koo, kongosho (pancreas), kifuko cha nyongo (gallbladder), kizazi, matiti (breast-cancer post-menopause) na figo.(WCRF/AICR 2007)

Si mara moja wala mbili bali ni mara nyingi nimewahi kusikia kutoka kwa watu mbalimbali wakisema “mimi sili lakini nanenepa tu” kwa kiasi kikubwa tafiti nyingi zinaonyesha hii sio kweli, kwa sababu uzito wa mwili ni uhusiano wa nishati-lishe (calories) inayoingia mwilini na ili inayotumika wakati viungo vya mwili vikifanya kazi.

Kwa maana hiyo huyu mtu anayeona yeye hali sana lakini ananenepa, uwezekano mkubwa ni kwamba anakula chakula kidogo lakini chenye nishati-lishe nyingi sana (labda kina mafuta au sukari kwa wingi), na uwezekano mwingine ni kwamba hali milo kamili kiasi cha kushiba mara moja bali anakula vitu vidogo vidogo mara kwa mara (snacks), kwa kiswahili tunaviita asusa. Basi kwa kuwa ni vidogo vidogo anajihesabu kuwa hukula chakula.

Tena mara nyingi kama sio mwangalifu asusa nyingi zinakuwa na mafuta au sukari sana. Na uwezekano mwingine ni kwamba anafanya kazi ambayo haitumii nguvu sana hivyo chakula anachokula kinahifadhiwa mwilini kama “unene”

Wakati mtu ambaye anafanya kazi ambayo haitumii nguvu sana anatakiwa kula vyakula ambavyo vitampa kiasi cha nishati-lishe kama kcal 2000 kwa siku, kuna baadhi ya vinywaji ambavo glass moja tu inampa mtu kcal. 1500. Mfano wa hivi ni kama baadhi ya mchanganyiko wa maziwa,cream na sukari (milk shake). Sasa kwa vyoyote mtu akinywa glasi moja atasema bado hajala kumbe ameshatumia nishati-lishe karibu kiasi ambacho kinahitajika kwa siku nzima. Kwa maneno mengine alitakiwa asile tena siku hiyo!!

Lakini kwa bahati mbaya sana kinywaji hicho hakina virutubisho vingine kwa uwiano ammbao unahitajika mwilini. Hapa ndipo tunatakiwa tujue namna ya kuchagua vyakula, kujifunza na kutaka kujua ndani ya chakula au kinywaji fulani kuna mchanganyiko gani na kwa kiasi gani. Pole pole ndio mwendo, tukijifunza tutajua namna ya kuwa waangalifu. Kwa vyakula vinavouzwa vikiwa na lebo, ni muhimu sana kujifunza kusoma lebo.

Najua si vema kuweka sheria kwamba acha kabisa kula chakula fulani, ila ni muhimu kuangalia kiasi na aina. Vipo vyakula ambavyo tunaweza kula kwa kiasi kingi kwa mfano mboga-mboga zisizo na wanga. Kuna aina ya vyakula ambavyo tunatakiwa kula kwa kiasi kidogo sana, kwa mfano vile vyenye mafuta mengi (kama. chipsi, mandazi, vitumbua, bagia, sambusa, ice-cream nk.), au sukari nyingi (kama. sukari, biskuti, cake, chokoleti, ice-cream, pipi, jamu, soda nk.).

Kula kwa kiasi ni muhimu. Kama unataka kuhakikisha uzito unapungua au hauongezeki punguza kiasi cha chakula unachokula. Kula ili kutuliza njaa na sio mpaka usikie tumbo limejaa! Fanya mazoezi ya mwili kama vile kutembea angalau dakika 30 kila siku.

Baadhi ya mambo ya kuzingatia katika kuhakikisha tunakula mlo ulio bora ni pamoja na, kula mbogamboga (zisizo na asili ya wanga) kwa wingi katika kila mlo, kutumia nafaka zisizokobolewa sana (relatively unprocessed cereals/grains) kila siku (kama dona, mchele wa brauni, ulezi, ngano isiyokobolewa sana), kutumia vyakula vinavyotokana na mimea kama sehemu ya mlo wako, kama vile aina mbali-mbali za maharage na mikunde, Kupunguza kiasi cha nyama hasa nyama nyekundu, na kuepuka matumizi ya nyama zilizosindikwa (kama soseji, bacon, nyama za kopo nk.).

Jipende! “Ufunguo wa Mtindo Bora wa Maisha upo Mkoni Mwako.

del.icio.us Digg Facebook Google Twitter Mail to a friend Thank you for sharing!
 Tagged as:
This entry was posted on Sunday, June 28th, 2009 at 5:30 am and is filed under Kiswahili, Lifestyle, Nutrition. You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0 feed. You can leave a response, or trackback from your own site.