Katika matunda yenye vitamin C kwa wingi, ubuyu ni mojawapo.  Tunda hili pamoja na virutubishi vingine, lina vitamin C kwa wingi sana lakini hata pale tunda hili linapopatikana halitumiki ya kutosha.  Tunapozungumzia “kula matunda kwa wingi kila siku”, ubuyu unaweza kuwa sehemu ya matunda hayo.  Pia ubuyu unaweza kutumika kutengeneza kinywaji kwa kutumia unga wake kuchanganya na maji yaliyo safi na salama.  Ubuyu pia unaweza kuchanganywa kwenye uji ambapo unaongeza ladha na virutubishi hasa vitamin C.

Tunda la ubuyu

Tunda hili wakati mwingine husahaulika na hata kudharauliwa, hasa pale linapopatikana kwa urahisi mno, na wakati mwingine hata bila kununua.  Kwa bahati mbaya sana matunda ambayo wakati mwingine tunayaita matunda pori, yameonekana kama matunda ya hali ya chini, au yasiyo na hadhi.  Hali hii tunahitaji kuibadili kwani tunda kama ubuyu au pia ukwaju na matunda pori mengine ni matunda mazuri sana, na inafaa tuyatumie kama sehemu ya matunda pale yanapopatikana, na hasa wakati wa msimu wake.

Tutumie matunda haya kutengeneza vinywaji kwa ajili ya familia.  Kutumia ubuyu pamoja na mlo husaidia kuongeza ufyonzwaji wa madini ya chuma kutoka katika chakula kilicholiwa hasa pale tunapotumia vyakula vitokanavyo na mimea.  Hii ni kwa sababu ubuyu una vitamin C kwa wingi, na vitamini C huhitajika ili kuongeza ufyonzwaji wa madini ya chuma kutoka kwenye mlo huo.  (Madini ya chuma huongeza damu mwilini).  Hivyo ni muhimu kwa kila mtu kufanya matunda  sehemu ya mlo, ukiwepo ubuyu, na hasa wanawake wajawazito ambao wana hatari kubwa zaidi ya kupata upungufu wa damu.

UBUYU…………..  tulienzi tunda hili! tulitumie! tuliongezee hadhi! Tulifaidi!  Tule matunda kwa wingi kila siku.

Jipende: Ufunguo wa mtindo bora wa maisha upo mkononi mwako.

Mti wa ubuyu

del.icio.us Digg Facebook Google Twitter Mail to a friend Thank you for sharing!
 Tagged as:
This entry was posted on Sunday, March 28th, 2010 at 2:09 pm and is filed under Kiswahili, Lifestyle, Nutrition. You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0 feed. Both comments and pings are currently closed.