Usafi na usalama wa chakula ni muhimu kwa kila mtu japo hapa namlenga zaidi mgonjwa wa saratani. Hii ni kwa sababu kinga ya mwili ya mgonjwa wa saratani imepungua kutokana na ugonjwa, kwa hiyo lazima ajitahidi sana kuzingatia usafi na usalama wa chakula. Pamoja na kutimiza kanuni zote za usafi wa mikono, vyombo, mazingira na maji ya kunywa, ni muhimu kuwa mwangalifu sana wakati tunapotayarisha au kutumia vile vyakula ambavyo kwa kawaida vina hatari kubwa zaidi ya maambukizi hasa ya magonjwa (hasa “salmonella”). Vyakula hivyo ni nyama yoyote mbichi (ikiwepo nyama ya kuku), mayai mabichi na samaki wabichi.
Kuepuka maambukizi ya magonjwa ni muhimu nyama ipikwe hadi kuiva (isiwe na dalili ya damu), na yai lisibaki la majimaji. Hii ni muhimu kwa kila mtu na ni muhimu zaidi kwa wagonjwa kama wa saratani kwani kinga ya mwili imepungua. Vyombo vinavyowekea nyama mbichi, samaki wabichi au kukorogea yai bichi vioshwe kwa maji na sabuni. Mikono ioshwe kwa maji yanayotiririka na sabuni mara tu baada ya kushika vyakula hivi vikiwa vibichi. Sehemu inayotumika kukatia nyama au samaki wabichi (kwa mfano kibao (cutting board)), isitumike kukatia vyakula ambavyo huliwa bila kupikwa (kwa mfano mkate au matunda). Daima kuwe na kibao maalumu cha kukatia nyama au samaki wabichi.
Unapokuwa mgonjwa ni muhimu pia kuepuka vyakula ambavyo hutengenezwa kwa kuongezwa mayai mabichi, kwa mfano mayonisi na baadhi ya “cheese cake”.
Mboga mboga zinazoliwa mbichi na matunda yaoshwe vizuri kwa maji safi yanayotiririka, chakula kilichohifadiwa kwenye friza kisiyeyushwe kwa kuachwa nje ya friza kwa muda mrefu, bali kiyeyushiwe ndani ya friji au kiyeyushwe kwa haraka kwa kuchemshwa moja kwa moja au kutumia ” microwave oven” kwa wale wenye microwave oven. Iwapo kiporo kinatumika kichemshwe hadi kuchemka kabisa hata kama kilikuwa kwenye friji. Ni muhimu pia kuepuka vyakula vilivyoota ukungu (fungus), kama nafaka au karanga zilizoota ukungu.
Jipende! Ufunguo wa mtindo bora wa maisha upo mkononi mwako






